Viongozi wa klabu za Barcelona (Hispania) na Gremio (Brazil), leo wanatarajiwa kukamilisha mazungumzo ya kumaliza dili la uhamisho wa kiungo Arthur Henrique Ramos de Oliveira Melo, baada ya kushindwa kufikia makubaliano mwezi Januari wakati wa dirisha dogo la usajili.
Pande hizo mbili zinakutana mjini Porto Alegre, Brazil na kuna matumaini makubwa ya kufikiwa kwa makubaliano kutokana na mchezaji husika, kuonyesha nia ya kutaka kucheza soka katika ligi ya nchini Hispania.
Katika mazungumzo ya leo Gremio watawakilishwa na rais wao Romildo Bolzan Jr na mtendaji mkuu Carlos Amadeo.
Endapo mambo yatakwenda kama yanavyotarajiwa, Arthur anatarajiwa kusafiri hadi mjini Barcelona juma hili kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya afya, na baadae kukamilisha uhamisho wake.
Tayari Gremio wameshatangaza tahamni ya kiungo huyo kuwa Euro milioni 30 sambamba na makubalino ya ziada ambayo yatafikiwa kwenye kikao cha leo.