Maafande wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT Tanzania) wamejizatiti kuibamiza Young Africans kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambao utachezwa leo jioni katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

JKT Tanzania ambao wana hali mbaya katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, watahitaji kushinda mchezo huo ili kujiondoa kwenye nafasi za chini katika msimamo wa ligi hiyo ambayo inaelekea ukiongoni.

Mkuu wa idara ya habari na mawasilino ya JKT Tanzania Jamila Mutabazi, amesema kwa mujibu wa Kocha Mkuu, Mohamed Abdallah Bares, morali wa wachezaji wao upo juu tayari kupambania alama tatu.

Amesema dhamira kubwa ya JKT Tanzania katika mchezo wa leo ni kupambana hadi dakika ya mwisho, ili kutimiza lengo la kuondoka na alama tatu, ambazo zitawasaidia kutimiza lengo la kujinasua kutoka kwenye nafasi ambazo ni hatarishi kwa timu yao.

“Japokuwa tunakutana na timu ambayo inashikilia nafasi ya juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu, kocha amesema haihofii kwa sababu tumejipanga vizuri kuhakikisha hatupotezi mchezo huo,” alisema Jamila.

Amesema mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na maandalizi yaliyofanywa na kila timu huku akiwaomba mashabiki wao wajitokeze kwa wingi uwanjani ili kuwapa hamasa wachezaji waweze kutimiza mipango yao.

Kikosi cha Young Africans kiliwasili mjini Dodoma jana asubuhi kikitokea jijini Dar es salaam, na jioni kilifanya mazoezi kwenye uwanja wa Jamhuri, ambao utatumika katika harakati za kusaka alama tatu za mchezo wa leo, kuanzia mishale ya saa kumi jioni.

Lamine, Ninja waachwa Dar
Mukoko Tonombe kuikosa JKT Tanzania