Kichapo cha mabao mawili kwa sifuri kilichotolewa na Dodoma Jiji FC katika mchezo wa mzunguuko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kimemfanya kocha mkuu wa JKT Tanzania Mohamed Bares, kujitokeza hadharani na kutoa kongole kwa matajiri yao ha ZABIBU.

Dodoma Jiji FC walipata ushindi wao wa pili mfululizo katika michezo ya Ligi Kuu ambayo wanayoshiriki kwa mara ya kwanza msimu huu, wakiwa ugenini kwenye uwanja wa Jamuhuri mjini Dodoma, mwishoni mwa juma lililopita, wakitangulia kuifunga Mwadui FC bao moja kwa sifuri Septemba 06.

Kocha Bares amesema kwa hakika Dodoma Jiji FC walionyesha soka safi na lenye kuvutia, hivyo walikua na kila sababu ya kumaliza dakika 90 wakiwa na alama tatu mkononi.

Kocha huyo akaongeza kuwa mbali na kutoa pongezi kwa wapinzani, pia kikosi chake kilionyesha kupambana, licha ya kuonyesha kasoro ndogo ndogo ambazo zilitoa nafasi kwa wageni wao kuzitumia na kuambulia ushindi wa mabao mawili kwa sifuri.

“Niwapongeze walicheza vizuri, na sisi pia tumecheza vizuri, lakini wenzetu walituzidi kwa kuwa yale makosa ambayo tumeyafanya wameweza kuyatumia,”

“Mpira ni mchezo ambao hautabiriki, leo tumecheza kadri ya uwezo wetu, lakini wenzetu wametuzidi kwa kutumia nafasi, yamepita na sasa tunasonga mbele,” alisema kocha huyo baada ya timu yake kukubali kipigo cha mabao mawili kwa sifuri katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma juzi.” amesema Bares.

Dodoma Jiji FC wataendelea na kampeni ya kusaka alama tatu za Ligi Kuu mwishoni mwa juma hili kwa kucheza Coastal union Jijini Tanga, huku JKT Tanzania wakitarajiwa kufunga safari kuelekea mkoani Kilimanjaro kupambana na mafande wa Jeshi la Polisi (Polisi Tanzania FC).

Masau Bwire: ‘KUPAPASA NA KUKUNG’UTA’
Bashiru awajibu wanaodai JPM ataongeza muda madarakani