Kocha Mkuu wa kikosi cha Tanzania Prisons Abdallah Mohamed Juma ‘Bares’ amesema, mipango mikubwa kwa sasa ni kuhakikisha kikosi chake kinasalia Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu ujao.

Bares ametoa kauli hiyo, baada ya Uongozi wa Tanzania Prisons kumthibitisha rasmi kwa kumsainisha mkataba wa mwaka mmoja akitokea Mlandege FC ya visiwani Zanzibar.

Bares amesema anatambua kazi aliyonayo klabuni hapo ni kubwa, lakini kwa ushirikiano wa wachezaji na maafisa wengine wa Benchi la Ufundi, anaamini watapambana na kuibakisha Ligi Kuu Klabu hiyo yenye maskani jijini Mbeya.

“Unajua sisi kama walimu kuna changamoto tunazipitia, unapofundisha timu za Ligi Kuu cha kwanza unapambania timu isishuke, hatupo katika nafasi nzuri, tupo tayari kwa mapambano”

“Naamini ushirikiano kutoka kwa wenzangu wa Benchi la Ufundi na Wachezaji utafanikisha malengo yaliyonileta hapa, Soka lina tabia ya kuleta matokeo ya furaha na huzuni, lakini nimedhamiria kuwapa furaha mashabiki wa Tanzania Prisons.” amesema Bares

Bares amechukua mikoba ya Kocha kutoka nchini Kenya Patrick Odhiambo, ambaye aliondoka klabuni hapo mwezi Januari, kufuatia mkataba wake kufikia kikomo.

Kwa mara ya kwanza Kocha Bares ataiongoza Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kesho Ijumaa (Februari 03), dhidi ya Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Robertinho: Tutashambulia tu
Serikali yasisitiza marufuku ya adhabu kali Shuleni