Wakala wa mshambuliaji wa pembeni wa mabingwa wa Hispania Real Madrid Gareth Bale, amesema mchezaji wake hana mpango wa kuachana na klabu hiyo ya mjini Madrid, licha ya kukabiliwa na changamoto ya kukosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza.
Bale amekua na wakati mgumu wa kuwa sehemu ya kikosi cha Meneja Zinedine Yazid Zidane, na hakubahatia kupangwa katika michezo yao saba ya mwisho, ambapo walifanikiwa kubeba taji lao la 34 la La Liga.
Hali hiyo ilimpa nafasi mshambuliaji wa zamani wa Tottenham Hotspur na Manchester United, Dimitar Berbatov kumshambulia Bale kwa kumwambia, amefanya si kama mwanasoka wa kulipwa baada ya kuigiza kulala akiwa benchi, huku timu yake ikicheza huku picha nyingine zilimwonyesha akiwa ameigiza kushika darubini.
Lakini, Jonathan Barnett wakala wa mshambuaji huyo kutoka Wales, amesisitiza kwa kusema “haendi kokote.”
Barnett amesema kwamba, Bale, anayelipwa Pauni 600,000 kwa juma, hataondoka kwa mkopo au kwa uhamisho wa jumla kama hakutakuwa na ofa nzuri kutoka kwenye klabu nyingine.
“Gareth yupo sawa tu. Ana miaka miwili kwenye mkataba wake. Anapenda kuishi Madrid, hivyo haendi kokote,” amesema Barnett.
“Bado mzuri kama ilivyo wachezaji wengine kwenye timu. Ni mambo ya Zinedine Zidane tu. Sawa, kuna timu zinamtaka, lakini ni ngumu kupata timu hapa duniani itakayoweza gharama zake. Ni huzuni kubwa kwamba hapati nafasi kwenye kikosi cha sasa cha Real Madrid, lakini hataondoka.”
Barnett amesema kwamba hakuna ugomvi wowote baina ya Zidane na Bale, lakini kocha huyo tu Mfaransa hataki kumchezesha. Zidane aliwahi kusema kwamba hana shida na Bale na kwamba alimwondoa kwenye timu katika mechi ya mwisho kutokana na mambo ya kiufundi tu.
Barnett aliwahi kumshambulia Zidane kwamba ni mtu wa hovyo kwa kumweka benchi Bale, mtu ambaye amefunga zaidi ya mabao 100 kwenye kikosi hicho cha Bernabeu.