Kampuni ya Barrick imetangaza kupunguza wafanyakazi zaidi ya 100 katika mgodi wa North Mara ili iweze kumudu gharama za uendeshaji.
Mgodi huo uliokuwa unamilikiwa na Acacia sasa hivi upo chini ya kampuni ya Twiga iliyoundwa kwa ubia wa serikali na Barrick Gold Corporation iliyokuwa kampuni mama ya Acacia.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa wafanyakazi mapema wiki hii, januari 13, 2020, uamuzi huo unatokana na tathimini iliyofanywa kubaini kama mgodi huo unawafanyakazi wenye taaluma zinazohitajika wakitekeleza majukumu yanayowahusu au la.
Sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa na meneja wa mgodi huo, Luiz Correia inasomeka “Kwa kuzingatia sheria ya nchi tunawajulisha wafanyakazi wote, na nakala tukiwa tumeipeleka Numet (Chama cha wafanyakazi mgodi wa North Mara) kuhusu dhamira hiyo”
kwa mujibu wa taarifa hiyo, upunguzaji huo utawahusu wafanyakazi 110 kutoka idara ya rasilimaliwatu, uchimbaji, usimamizi wa mali pamoja na ugavi.
wengine watakaoathirika ni kutoka idara ya uhandisi mitambo, huduma kwa jamii, mazingira na usalama kazini.
Meneja Correia amesema mchakato huo utazingatia sheria zote za nchi kuhakikisha kila anayeguswa anapata stahiki zake hivyo amewaasa wafanyakazi kuwa watulivu na kuendelea na majukumu yao.