Kampuni ya Barrick ambayo imetenga kiasi cha dola milioni 300 (zaidi ya bilioni 700) kwa ajili ya kuilipa Serikali ya Tanzania kuonesha uaminifu, imeweka sharti la kuruhusiwa kusafirisha Makinikia yaliyozuiwa bandarini.

Mwezi Machi, Serikali ilizuia usafirishwaji wa mchanga wenye madini (makinikia) uliokuwa unasafirishwa na kampuni ya Acacia ambayo ni kampuni tanzu ya Barrick. Ripoti maalum ilionesha kuwa mchanga huo ulikuwa na kiwango cha madini mara kumi zaidi ya kile kilichoanishwa na Acacia.

Barrick kupitia taarifa yake ya miezi mitatu (Julai-Septemba) iliyotolewa wiki hii, imeeleza kuwa kutokana na kushikiliwa kwa mchanga huo, pamoja na mambo mengine, imepata hasara ya dola milioni 11 (zaidi ya shilingi bilioni 24), ambayo ni tofauti na faida ya dola milioni 175 (zaidi ya shilingi bilioni 385) waliyoipata katika kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Hivyo, Barrick wameiomba Serikali kuruhusu mchanga huo kusafirishwa huku wakieleza kuwa kiasi hicho cha fedha kitalipwa kwa awamu na kwa kutegemea hali ya uzalishaji na pato la Acacia.

“Kuyumba kwa mapato kunatokana na kushuka kwa uzalishaji na bei ya dhahabu pamoja na zuio la kusafirisha makinikia ambalo Serikali ya Tanzania iliiwekea Acacia,” taarifa hiyo imeeleza.

Aidha, Barrick wameeleza kuwa wanaendelea kufanya mazungumzo na Serikali kuhusu deni la shilingi trilioni 424 kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), na kwamba mazungumzo hayo ambayo pia yatahusisha ombi la kuruhusu kusafirisha makinikia yanaweza kukamilika katika nusu ya mwaka ujao.

Trump aanika nyaraka za upelelezi wa mauaji ya ‘Rais Kennedy’
Magazeti ya Tanzania leo Oktoba 27, 2017