Barua iliyoandikwa na Rais wa Marekani, Donald Trump, ikisifu ushirikiano kati ya Marekani na mataifa ya Afrika, imepokelewa kwa hisia tofauti na viongozi wa bara hilo wanaohudhuria mkutano wa 30 mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Katika barua hiyo, Trump amesema kuwa anaiheshimu Afrika na atamtuma waziri wake wa mambo ya nje, Rex Tillerson kutembelea mataifa kadhaa kuanzia mwezi Machi mwaka huu.

Amesema kuwa White House itawaalika baadhi ya viongozi kutoka bara la Afrika katika juhudi za kuimarisha uhusiano huo uliopo na kuangalia namna gani ya kuweza kuuendeleza.

“Marekani inayaheshimu sana mataifa ya Afrika na raia wake, Wanajeshi wetu wanafanya operesheni kwa kushirikiana na wale wa Afrika, ni wakati wa kuimarisha na kudumisha uhusiano wetu,” barua hiyo ilisema.

Aidha, hayo yanajiri huku baadhi ya viongozi wa Afrika wakiendelea kumtuhumu rais huyo, kufuatia kauli aliyoitoa kuwa mataifa ya Afrika na Haiti ni machafu.

Wakati huo huo, Katibu mkuu wa umoja wa mataifa, Antonio Guterres, ameahidi kushirikiana zaidi na bara la Afrika na kusema kuwa Umoja huo utakuwa ni msaada zaidi katika kuimarisha suala la usalama.

Hata hivyo, Mkutano huo wa 30 unatarajiwa kujibu barua iliyoandikwa na rais Trump kufuatia tuhuma kwamba alitumia maneno ya kudhalilisha yaliyowalenga wahamiaji kutoka mataifa ya Kiafrika pamoja na wale wa kutoka Haiti.

 

Video: Polepole avunja ukimya Lissu kupigwa risasi, Rafu za uchaguzi zaanza Kinondoni
Magazeti ya Tanzania leo Januari 29, 2018