Timu ya soka ya Borussia Dortmund jana usiku ilipata pigo baada ya kushambuliwa na milipuko mitatu muda mfupi kabla ya mchezo wake wa robo fainali ya Kombe la Mabingwa barani Ulaya dhidi ya Monaco ya Ufaransa.

Jeshi la polisi la Dortmund kupitia mkutano na waandishi wa habari ulioongozwa na mkuu wa jeshi hilo wa Dortmund lilieleza kuwa milipuko yote mitatu ilikuwa imeilenga timu hiyo.

Hata hivyo, milipuko hiyo haikulipata moja kwa moja basi lililokuwa limebeba wachezaji lakini kishindo cha mlipuko kilipelekea vioo vya gari hilo kuporomoka na matairi kupasuka, huku mchezaji Marc Bartra akiripotiwa kupata majeraha katika eneo la kiuno na mkononi.

Marejaha ya Bartra yametokana na vioo vilivyoruka na kumshambulia katika maeneo ya mwili wake na kupelekea kufanyiwa upasuaji.

Mwendesha mashtaka wa serikali ameeleza kuwa kuna barua ambayo ilikutwa karibu na eneo la tukio hilo na kwamba uchunguzi unaendelea dhidi yake.

Akieleza kwa ufupi, amesema barua hiyo ilikuwa inaeleza kuhusu uhusika wa shambulizi dhidi ya timu hiyo, ikiaminika kuwa imetoka kwa wapangaji wa tukio hilo.

Kadhalika, polisi wamedai kuwa wamepata vitu vinavyoweza kuunganishwa kwenye tukio hilo vikiwa katika hoteli ambayo timu hiyo ilifikia.

Kutokana na tukio hilo baya, mchezo kati ya Dortmund na Monaco uliahirishwa hadi Jumatano.

Wakati tukio hilo likitokea, tayari mashabiki zaidi ya 80,000 walikuwa ndani ya uwanja wakisubiri mtanange huo, ambapo Jeshi la polisi liliwaomba kutoondoka hadi hali itakapokuwa shwari. Baada ya muda wote waliondolewa wakiwa salama.

Raia wa Dortmund walieleza kufurahishwa na ushirikiano uliooneshwa na mashabiki wa Monaco, hali iliyopelekea kuwakarimu wakiwaalika kupitia mitandao ya kijamii kuwa wangewapa malazi kwa usiku huo.

 

 

Jafo awanyooshea kidole watumishi wa umma, awataka kujirekebisha
Live: Yanayojiri Bungeni Dodoma muda huu