Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) limesitisha usajili wa msanii Godfrey ‘Dudu Baya’ Tumaini kwa kile walichoeleza kuwa ni utovu wa nidhamu.
Kupitia barua yake ya Februari 28 mwaka huu, Basata wameeleza kuwa wamefikia uamuzi huo baada ya msanii huyo kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kutoa kauli zisizofaa kwenye mitandao ya kijamii.
“Baraza linasisitiza kuwa msanii anaposajiliwa anapaswa kuwa raia mwema na mfano wa kuigwa na jamii kwa kuzingatia msanii ni kioo cha jamii na sio vinginevyo,” imeeleza sehemu ya barua hiyo Iiliyosainiwa na Katibu Mtendaji, Godfrey Mngereza.
Hivi karibuni, Dudu Baya aliweka kwenye Instagram vipande vya video ambavyo vilimuonesha akitoa lugha zisizofaa dhidi ya marehemu Ruge Mutahaba, aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group. Kitendo hicho kililaaniwa na watu wengi.
“Basata inaungana na Wasanii na Watanzania wote waliojitokeza kukemea kitendo cha Msanii Dudubaya ambacho hakifai, hakikubaliki na hakiendani na Utamaduni wa Mtanzania,” imeeleza Basata.
Jeshi la Polisi lilimkamata na kumshikilia katika kituo cha Oysterbay jijini Dar es Salaam kufuatia agizo la Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe kwa jeshi hilo pamoja na Basata.