Sakata la dawa za kulevya limetikisa Bunge mjini Dodoma baada ya wabunge kutaka orodha ya wauza unga ambayo Rais mstaafu Jakaya Kikwete alisema anayo ili ifanyiwe kazi na mrithi wake, Rais John Magufuli.
Akichangia taarifa za Kamati ya Bunge ya Ukimwi na Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe amesema Rais Kikwete aliwahi kutangazia umma kuwa anayo orodha ya vigogo wa dawa za kulevya hivyo ametaka wakamatwe ili watumiaji waachiwe.
“Kikwete alisema anayo orodha ya wauza dawa za kulevya. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi amfuate kule Msoga ili ampe hiyo orodha. Naamini watumiaji wataachiwa, Vita ya dawa za kulevya siyo ya Paul Makonda, hii ni vita ya Serikali na naamini itamuunga mkono. Mtu akipimwa akionekana ni mtumiaji atusaidie kumpata muuzaji,” amesema Bashe.
Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee amemtaka Rais Magufuli kuacha kuendesha nchi kwa sanaa na kutafuta habari zake zipewe uzito katika vyombo vya habari, badala ya kushughulika na tatizo.
Mbunge huyo amesema kwa mwaka 2016/2017, Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini ambayo ndiyo yenye dhamana ya vita hiyo haikupata fedha za maendeleo.
Aliongeza, “Vita hii inahitaji utashi wa kisiasa. Kikwete alisema anawajua wauza unga kwamba ana orodha. Alipoondoka Ikulu si aliacha mafaili? Orodha unayo hapo Ikulu tusicheze na akili za Watanzania,” alisema