Mbunge wa Nzega Mjini kupitia Chama Cha Mpinduzi (CCM), Hussein Bashe amesema kuwa hajafurahishwa baada ya yeye, Januari Makamba pamoja na Mbunge wa Mtama Nape Nnauye, kutajwa kuwa miongoni mwa watu ambao washajiunga na chama cha ACT – Wazalendo na wanasubiri kipindi cha Ubunge kiishe.
Ameyasema hayo kupitia ukurasa wake wa Twitter baada ya mtu anayedaiwa kudukua mawasiliamo ya Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kuchapisha taarifa juu ya Wabunge hao kujiunga na ACT – Wazalendo muda wowote.
Mdukuzi huyo ameandika kuwa anawakaribisha pia Hussein Bashe na Nape Nnauye ambao tayari wameshachukua kadi za uanachama wa ACT- Wazalendo na wanachosubiri ni kuvunjwa kwa bunge na bila kumsahau mdogo wake Januari Makamba.
Akijibu madai hayo Mbunge wa Nzega Hussein Bashe ameandika kuwa wanaofahamu siasa za Tanzania na wanaofahamu vizuri misimamo ama maamuzi yake ya kisiasa, huwa hafanyi kwa njia za kificho, na siku akiamua kuondoka CCM ataondoka hadharani wala hatasubiri njia za kificho.
”Hili Genge la kihuni ambalo linaongozwa na wahuni wachache ipo siku nitawataja kwa majina, ila mpango wenu wakutaka kunifanya nione CCM si chama sahihi kwa mimi kuwatumikia wananchi wa Nzega na Tanzania hautafanikiwa,CCM bado nipo sana,” ameandika Bashe kwenye ukurasa wake wa kijamii.