Basi la klabu ya Hertha Berlin inayoshiriki ligi daraja la kwanza nchini Ujerumani limepigwa risasi kwenye kioo na mtu asiejulikana wakati likiwa safarini.

Mkasa huo umetokea kaskazini magharibi mwa nchini Ujerumani ambapo kikosi cha Hertha Berlin kimekwenda kwa ajili ya kucheza mchezo wa kombe la chama cha soka nchini humo DFB dhidi ya Arminia Bielefeld.

Inadaiwa kwamba, mtu mmoja aliyekua kwenye pikipiki ndiye aliesababisha tukio hilo kwa kupiga risasi kwenye kioo cha basi la klabu hiyo ya ligi kuu ya nchini Ujerumani.

Mtu huyo alilipita basi hilo na kufanya kitendo hicho ambacho hakikumdhuhuru yoyote na wala hakikupasua kioo chote zaidi ya kuonekana ufa.

Hata hivyo kwenye basi hilo hakukuwa na watu zaidi ya dereva aliyekua akielekea hotelini ambapo timu ilikua imefikia kwa ajili ya kuwapeleka sehemu ya kufanyia mazoezi.

Uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea kufanywa na mamlaka za kiusalama nchini Ujerumani.

 

TWIGA STARS YAENDELEA KUJIFUA ZANZIBAR
TP Mazembe Kuwasajili Watanzania Wengine