Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Cameroon Clarence Seedorf amemuita mshambuliji Christian Bassogog, kwa mara ya kwanza tangu alipokabidhiwa kikosi cha timu hizo miezi kadhaa iliyopita.
Wakati akitangaza kikosi kilichocheza mchezo ya kuwania kufuzu fainali za Afrika mwezi huu dhidi ya Comoro, Seedorf alimuacha mshambuliaji huyo ambaye alikua miongoni mwa wachezaji waliounda kikosi kilichotwaa ubingwa wa Afrika mapema mwaka 2017 nchini Gabon.
Seedorf, amesema maamuzi ya kumuita kwa mara ya kwanza Bassogog yamekuja baada ya kumfuatilia akicheza katika klabu yake ya Henan Jianye inayoshiriki ligi kuu ya China, na amejiridhishwa anamfaa, katika mchezo wa mwezi ujao dhidi ya Malawi.
Hata hivyo kocha huyo kutoka nchini Uholanzi amemtema aliyekua nahodha wa kikosi cha Cameroon Benjamin Moukandjo, ambaye pia anacheza katika ligi kuu ya China.
Hatua ya kuachwa kwenye kikosi cha Cameroon kitakachocheza mchezo dhidi ya Malawi mwezi ujao, imemfanya mchezaji huyo kutangaza kustaafu kuitumikia timu ya taifa.
Benjamin Moukandjo
Hii si mara ya kwanza kwa Moukandjo kuachwa na kocha Seedorf, kwani hata katika mchezo wa mwezi huu dhidi ya Comoro uliomalizika kwa sare ya bao moja kwa moja, hakuitwa kikosini.
Moukandjo alikiongoza kikosi cha Cameroon katika fainali za Afrika mwaka 2017, na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Afrika kwa kuifunga Misri kwenye mchezo wa fainali mjini Brazzaville nchini Gabon.