Kiungo Bastian Schweinsteiger, ametangaza kustaafu kuitumikia timu ya taifa ya Ujerumani, ikiwa ni majuma kadhaa baada ya timu hiyo kushindwa kufikia malengo ya kutwaa ubingwa wa barani Ulaya.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 31, alikuwa sehemu ya mafanikio yaliyopatikana wakati wa fainali za kombe la dunia za mwaka 2014, ambapo Ujerumani walitwaa ubingwa wa fainali hizo katika ardhi ya Brazil kwa kuifunga bao moja timu ya taifa ya Argentina.

Schweinsteiger, ametangaza kustaafu soka la kimataifa huku akiacha kumbu kumbu ya kuitumikia timu ya taifa ya Ujerumani katika michezo 120 sambamba na kufunga mabao 24.

“Katika michezo 120 niliyocheza nikiwa na timu yangu ya taifa, sina budi kujivunia kwa mafanikio niliyoyapata na ninaamini kipindi hiki ni sahihi kwangu kutangaza kuachana na timu hiyo, ili kupisha wachezaji wengine,”Imeeleza taarifa ya Schweinsteiger.

Schweinsteiger, alikabidhiwa jukumu la kuwa nahodha wa kikosi cha Ujerumani, mara baada ya Philipp Lahm kutangaza kustaafu soka la kimataifa siku chache baada ya fainali za kombe la dunia za mwaka 2014.

Ataendelea kukumbukwa kwa mchango wake alioutoa wakati wa fainali za kombe la dunia za mwaka 2006 ambapo Ujerumani walimaliza katika nafasi ya tatu, fainali za mwaka 2010 – Ujerumani wakishika nafasi ya tatu na fainali za mataifa ya barani Ulaya (Euro 2008) Ujerumani wakimaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Hispania.

Aliwahi kutajwa katika kikosi cha wachezaji waliofanya vyema wakati wa fainali za kombe la dunia za mwaka 2010 na kuunda kikosi cha dunia (FIFA World Cup Dream Team 2010).

Video: Polisi Dar wakamata magari yaliyoibiwa
Video: Jambazi hatari auawa, Akutwa na bastola aina ya Glock17 na risasi sita