Baraza la Vijana Chadema (BAVICHA) limeeleza kuwa halina chuki yoyote na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli bali wanampenda na wanachofanya ni kumsaidia kuwa bora.

Mwenyekiti wa BAVICHA, Patrobas Katambi ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipofanya mkutano na waandishi wa habari kuhusu azimio lao la kufanya maandamano nchi nzima Septemba 1 mwaka huu, kutekeleza operesheni wanayoiita Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (UKUTA).

“Tunapomtoa dosari na kasoro haimaanishi kuwa sisi tunamchukia Rais Magufuli. Tunamtoa dosari na kasoro maana yake tunamsaidia Rais ili aweze kujirekebisha kwenye mambo kadha wa kadha na kuwasaidia watu wake wa chini kuongoza vizuri,” alisema Katambi.

Aidha, Mwenyekiti huyo wa BAVICHA alitoa wito kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu kuandaa jeshi lake kwa ajili ya kulinda mikutano na maandamano ya UKUTA, kama walivyoulinda Mkutano Mkuu Maalum wa CCM.

Alisema kuwa nia ya chama hicho ni kufanya mikutano na maandamano kwa amani bila kuvunja sheria.

Rais ataja majina ya wauza ‘Unga’, wamo majaji, wabunge
Oscar Pistorius akimbizwa hospitali baada ya kupata majeraha Jela