Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), limeshtushwa kutajwa kwa Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe kwenye vita dhidi ya dawa za kulevya ambapo wamesema kuwa kitendo hicho ni cha kumchafua na kumkwamisha kiuchumi.
Kauli hiyo ya Baraza hilo imetolewa na Katibu Mwenezi wa Bavicha, Edward Simbeye baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda kutaja orodha ya majina 65 ya watuhumiwa wa dawa za kulevya akiwemo Mbowe.
Simbeye amesema kuwa mbali na kumchafua pia ametumwa kuhakikisha wanakamilisha mwendelezo wa mkakati maalumu wa kuangamiza upinzani kabla ya mwaka 2020.
“Huko kote Makonda anazunguka tu, ila kinachotafutwa kwa Mwenyekiti wetu tulikitarajia na kwa sasa adui anafikia eneo ambalo tunalolisubiri kwa hamu sana, ili tushughulikiane vizuri kisheria,”amesema Simbeye.
Hata hivyo Simbeye amesema kuwa anachokifanya Makonda si cha kubahatisha ila ni kwa mpango maalumu na kwamba amekuwa Mkuu wa Mkoa wa Taifa kutokana na mambo mengi anayoyazungmza si ndani ya mkoa wake tu na hata mikoa mingine.