Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) limetangaza kufunga ofisi zake zilizopo nchini Burundi pamoja na shughuli zake zote nchini humo baada ya juhudi za kupata suluhu na serikali kushindikana.
Mwezi machi mwaka huu, Baraza la Kitaifa la Mawasiliano nchini Burundi lilipiga marufuku matangazo ya mashirika mawili ya utangazaji ambayo ni BBC na Sauti ya Amerika (VOA) nchini humo na watu kukatazwa kutoa taarifa ya aina yeyote baada ya mashirika hayo kutuhumiwa kurusha matangazo ambayo serikali ilidai yamechafua sifa ya nchi.
Baraza hilo lilisema kuwa halimruhusu mwandishi yeyote, awe raia wa Burundi ama yule wa kigeni kutoa habari yoyote kwa mashirika hayo ya habari.
Aidha, amri hiyo ilitokana na kile kilichoitwa na mamlaka, kuwa makala ya uongo ya BBC iliyotolewa mwaka uliopita kuhusu mauaji yaliyotekelezwa na vikosi vya usalama katika nyumba ya siri ndani ya mji mkuu wa Bujumbura.
Hata hivyo, serikali ya Burundi imesema kuwa makala hiyo ilikiuka sheria za habari nchini humo., huku BBC ikiendelea kusisitiza kuwa makala hiyo ilifuata taratibu zote za kiuandishi na kutetea waandishi wake.