Kocha wa Ivory Coast Patrice Beaumellle amesema Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’ linaua soka la Afrika, kwa kuendelea kubariki nafasi tano za ushiriki kwenye Fainali za kombe la Dunia.
Kocha huyo kutoka nchini Ufaransa ametoa kauli hiyo, baada ya kikosi chake kushindwa kupata nafasi ya kuendelea kwenye mchakato wa kusaka nafasi ya kusaka nafasi ya kushiriki Fainali za Kombe la dunia 2022, zitakazounguruma nchini Qatar.
Ivory Coast ilipoteza mchezo wa mwisho dhidi ya Cameroon kwakukubalia kufungwa bao 1-0, na kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi D kwakufikisha alama 13.
Cameroon imemaliza kinara wa kundi hilo, kwa kufikisha alama 15, hivyo nchi hiyo inakuwa sehemu ya mataifa kumi yatakayocheza hatua ya mwisho ya mtoano.
Kocha huyo amesema Afrika ina nchi 54 zilizoshiriki kuelekea Fainali za Kombe la Dunia zinazoshirikisha mataifa 32, lakini cha ajabu bara hilo linaendelea kupewa nafasi 5.
Wakati bara la Ulaya lenyewe lina uhakika wa nafasi 13 kutoka timu 55 na Amerika ya Kusini wana nafasi nne za uhakika kutoka timu 10.
“Ni jambo la aibu kwasababu timu imara kama ya kwangu itasalia nyumbani,”aliendelea kusema kocha huyo mfaransa Beaumelle.
“Nimekuwa ndani ya Afrika tokea 2008 na nimeweza kushiriki michezo mbalimbali ya kufuzu kombe la dunia.
“Nataka kuzungumza na FIFA kwa sababu unapoona ya kwamba tuna mashirikisho 54 na ni tano pekee wanaokwenda kombe la dunia ni majanga”
“Sipo kwaajili ya kulaumu mabara mengine, lakini FIFA wanauwa soka la Afrika.
“Ni aibu kuwa na wachezaji wakubwa ambao mabingwa wa soka la Ulaya huwa wanajivunia, lakini hawawezi kwenda kushiriki kombe la Dunia”