Rais wa zamani wa Ivory Coast, Henri Konan Bedie, mmoja wa wanasiasa wakongwe waliotawala katika taifa hilo la Afrika magharibi, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 89.
Bedie alihudumu kama rais kuanzia mwaka 1993 hadi alipoondolewa madarakani mwaka 1999 na baadaye akagombea urais ambao alishindwa dhidi ya mpinzani wake wa muda mrefu, Rais Alassane Ouattara katika uchaguzi wa 2020.
Atakumbukwa kwa jukumu lake katika kukuza suala la “ivoirite” (utambulisho wa Ivory Coast), ambalo lilichochea mvutano kati ya wale wanaojiona kuwa wenyeji wa kusini na mashariki, na wafanyakazi wengi wa kigeni kutoka nchi jirani.
Hata hivyo, akiwa Rais, Bédié alihimiza uthabiti wa kitaifa japo alishutumiwa kwa ukandamizaji wa kisiasa na ufisadi ambapo pia katika uchaguzi wa urais Oktoba 1995, alirekebisha kanuni ya uchaguzi ili kuwataka wagombea urais wawe wamezaliwa na wazazi wawili wa Ivory Coast na wameishi nchini humo kwa miaka mitano kabla ya uchaguzi iliyomlenga mpinzani wake Ouattara.