Bei ya mafuta ya kupikia nchini imepanda kufuatia kuadimika kwa bidhaa hiyo ambapo sababu kubwa imetajwa kuwa ni kukamatwa kwa meli kubwa mbili zenye mafuta ya kupikia mpaka wamiliki hao watakapolipa kodi.
Sakata la kuzuia meli hizo mbili zenye tani 62,00 za mafuta ya kula katika bandari ya Dar es salaam limepelekea upatikanaji hafifu wa mafuta nchini na kusababisha gharama za mafuta kuwa ghali.
Ambapo kwa taratibu zilizopo mafuta safi ya kula yanayoingizwa kutoka nchi za nje hulipiwa kodi ya asilimia 25 wakati ghafi yanatozwa kwa asilimia 10.
Aidha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameahidi kusimamia swala hilo huku Mkurugenzi wa Elimu ya Mlipa kodi wa TRA, Richard Kayombo amesema hakuna namna nyingine zaidi ya wamiliki wa meli hizo kulipa kodi husika badala ya kuenedelea kulalamika.
”Ni kweli tunazishikilia meli mbili zenye mafuta ya kupikia, wanachotakiwa kufanya ni kulipa kodi tu, kama wanaona wameonewa wafuate taratibu wa kukata rufaa siyo kulalaimka kwenye vyombo vya habari amesema Kayombo.
Aidha uchunguzi uliofanywa unaonyesha maeneo mbalimbali ya nchi bei ya mafuta imepanda kwa kasi na kuadimika na kwamba nchi ina uwezo mdogo wa kuzalisha mafuta kulinganisha na uhitaji ambapo uhitaji ni tani 570,000 wakati uzalishaji nchini ni tani 210,000 hivyo kuna uhitaji mkubwa wa mafuta kutoka nje ili kukidhi uhitaji wa wananchi wote nchini.