Serikali inatarajia kutangaza bei mpya za vifurushi vya simu mwisho mwa mwezi huu, ili kila mtanzania amudu kuvitumia na kupata huduma bila tatizo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye wakati akizindua mnara uliojengwa na mfuko wa mawasiliano kwa wote kwa kushirikiana na kampuni ya Vodacom, katika kijiji cha Kinenulo kilichopo kata ya Imalinyi, wilayani Wanging’ombe mkoani Njombe.
Nape, amesema Serikali inakamilisha mapitio ili kuona namna ya kusaidia kupunguza gharama ili mwananchi wa kawaida apate huduma bila tatizo.
“Kwa kuzingatia hilo na ilani ya uchaguzi ya CCM, tumetakiwa kuwafikia zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania, hivyo kujenga mnara pekee kama mtu hawezi kuutumia utakuwa hauna maana,” amesema Nape.
“Mtu wa kawaida kununua simu ya Sh300,000 ni ngumu kidogo, lakini tukimwambia weka elfu thelathini upewe simu ya laki tatu, atakuwa anakatwa kidogokidogo hata kama ni kwa mwaka mzima itawezekana,”
Naye Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Justina Mashiba amesema Mkoa wa Njombe una jumla ya miradi ya ujenzi wa minara 32, ambapo 30 kati ya hiyo imekamilika na miwili ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji, ikigharimu Sh4.8 bilioni.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka aliipongeza UCSAF kwa namna ambavyo wamekuwa wadau wakubwa wa maendeleo kwenye sekta ya mawasiliano na Serikali, hususani kwenye maeneo ya vijijini.