Kumekuwa na mfumuko mkubwa wa bei hasa katika kipindi hiki kuelekea sikukuu ya Eid El-Hajj ambayo itaswaliwa kesho Jumatano ya Agosti 22, 2018.
Ambapo katika masoko mbalimbali ya mifugo jijini Dar es salaam hasa soko la Pugu ng’ombe aliyekuwa akiuzwa kwa Sh 600,000 amepanda na kufikia hadi Sh Milioni 1.2 na kupelekea kilo 1 ya nyama kuuzwa 6500 toka 6000 huku mbuzi kutoka sh 120,000 hadi 200,000 na kuku kutoka 10,000 hadi 12,000 na kuku wa kienyeji toka 18,000 hadi 20,000.
Na nyanya zimeshuka kutoka 50,000 kwa kasha hadi kufika sh 25,000 huku zilizolala zikiwa sh 18,000.
Kupanda kwa bei hizo kunatokana na uzito wa sikukuu ya Eid ya kuchinja ambako Waislamu wengi huchinja kwa lengo la kutimiza moja ya nguzo za uislamu.
Katika eneo la vinginguti ambako huuzwa mbuzi kwa wingi mifugo hao wanauzwa kati ya sh 175,000 hadi 200,000.
Mmoja wa wafanyabiashara katika eneo hilo, khasimu Said alisema bei hiyo imepanda kutokana na mahitaji ya mbuzi kuwa makubwa huku wafugaji wakiuza mifugo kidogo.
”Bei zimepanda kwa sababu wakulima wamepata chakula cha kutosha hivyo hawana mahitaji wa kuuza zaidi mifugo yao,” amesema Said.
Aidha Meneja wa soko la Ilala, Selemani Mfinanga amesema katika soko hilo wanatarajia kuongezeka zaidi kwa bei za bidhaa nadani ya siku hizi mbili kutokana na maandalizi ya Sikukuu ya Eid.