Beka Flavour amefunguka  kuwa  hayupo tayari kurudi kwenye kundi la Yamoto Band endapo ikitokea wanatakiwa kurudisha Kundi na kufanya kazi pamoja kama ilivyokuwa awali.

Msanii huyo ametaja maslahi kuwa moja kati ya changamoto kubwa ambazo alikutana nazo kwenye kundi hilo na kwamba hawakuwa wanapata fedha zinazoendana na kazi waliyokuwa wakifanya.

Amesema kuwa wakati wanaondoka kwenye kundi hilo hawakuwa na pesa zozote kwani wakati wanafanya matamasha mbalimbali walikuwa wanapewa fedha za matumizi tu. Aliongeza kuwa wao walipendekeza kwa uongozi fedha zinapopatikana wafanyiwe mambo kadhaa ikiwa pamoja na kujengewe nyumba.

“Mimi sasa hivi ukisema nitoke kwenye uongozi wangu mpya nirudi Yamoto Band sidhani kama itawezekana!” Beka aliiambia Planet Bongo ya East Africa Radio.

“Unajua watu hawajui tu lile kundi ndiyo limekufa tayari kwa sababu sasa hivi kila msanii yupo na uongozi wake, sidhani kama wanaweza kukubaliana watoke walipo na kurudi kule,” aliongeza.

Katika hatua nyingine, Beka ameeleza kufurahishwa na namna ambavyo aliyekuwa mwanafamilia mwenzake wa Yamoto Band, Aslay anavyofanya vizuri.

“Mimi nazidi kumuombea kwani mwenzangu amekuwa kati ya wasanii ambao wanazungumziwa sana kutokana na kazi zake, lakini napenda kuwaambia Watanzania kuwa wasanii ambao tulikuwa tunaunda kundi la Yamoto Band Mungu alitupa kitu ndani yetu. Hivyo, muda si mrefu mtakuja kuona  haya nayosema kwani kila mmoja ana upekee wake katika kazi zake,” alifunguka.

Mahaba Niue: Huddah amfungukia Jux
Video: Zitto Kabwe amvaa Prof. Kabudi kuhusu makinikia