Mchezaji wa timu ya Singida United, Shafik Batambuze amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Septemba wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2017/2018.
Batambuze anayecheza nafasi ya ulinzi wa pembeni, alitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili, Ibrahim Ajibu wa Yanga na kiungo Mohammed Issa wa Mtibwa Sugar, alioingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam.
Uchambuzi huo kwa mujibu wa utaratibu hufanywa na kikao cha Kamati ya Tuzo ya VPL inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutokana na mapendekezo kutoka kwa makocha waliopo viwanja mbalimbali ambavyo ligi hiyo inachezwa msimu huu.
Mchezaji huyo alitoa mchango mkubwa kwa Singida United kupata pointi 10 katika michezo minne, ambayo timu yake ilicheza kwa mwezi huo, matokeo ambayo yaliiwezesha Singida United kutoka nafasi ya 10 katika msimamo na kupanda hadi nafasi ya nne kwa mwezi huo wa Septemba. Singida United ndiyo timu iliyokusanya alama nyingi kwa mwezi huo ukilinganisha na timu nyingine 15 zinazoshiriki VPL.
Singida United iliifunga Mbao FC mabao 2-1 Uwanja wa Jamhuri Dodoma, ikaifunga Stand United bao 1-0 Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, iliifunga Kagera Sugar Uwanja wa Jamhuri Dodoma na ilitoka sare ya bao 1-1 na Azam FC uwanja huo huo. Michezo yote hiyo Batambuze alicheza dakika zote 90 kwa kila mchezo, ambayo ni sawa na kucheza dakika 360.
Kwa upande wa Ibrahim Ajibu alitoa mchango mkubwa kwa Yanga uliowezesha kupata pointi nane kwa mwezi huo, baada ya kushinda michezo miwili na kutoka sare miwili, ambapo pia Mohammed Issa aliisaidia timu yake kupata pointi nane katika michezo minne iliyocheza mwezi huo, ikishinda miwili na kutoka sare miwili.
Kampuni ya Vodacom, ambao ndiyo wadhamini wa ligi hiyo ina utaratibu wa kuwazawadia wachezaji bora wa kila mwezi, huku pia mwisho wa msimu kukiwa na tuzo mbalimbali zinazohusu ligi hiyo, ambapo msimu wa mwaka 2016/2017 kulikuwa tuzo 16 zilitolewa kwa washindi wa kada mbalimbali. Batambuze atazawadiwa Sh milioni moja kwa kuibuka Mchezaji Bora wa mwezi.