Beki wa Mabingwa wa Soka Barani Afrika Wydad AC, Arsène Zola Kiaku amefunguka kuelekea mchezo wa Mkondo wa Pili wa Robo Fainali, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Simba SC.

Mchezo huo utapigwa baadae leo Ijumaa (April 28) katika Uwanja wa Mohamed V mjini Casablanca nchini Morocco kuanzia saa nne usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Zola ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha Wydad AC kilichoikabili Simba SC jijini Dar es salaam Jumamosi (Aprili 22), katika Uwanja wa Benjamin Mkapa amesema wanawaheshimu wapinzani wao kutoka Tanzania, kwa kuwa wana kikosi kizuri.

Beki huyo kutoka DR Congo amesema wamejiandaa vizuri kukabiliana na Simba SC, na kikosi chao kina hamasa kubwa kuelekea mchezo huo, ambao unatarajiwa kuhudhuriwa na mashabiki wengi wa soka mjini Casablanca.

“Tunaiheshimu Simba SC kwa kuwa ina kikosi bora na kizuri, kilitupa upinzani mkubwa katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza tuliocheza Tanzania juma lililopita, katika mchezo wa Mkondo wa Pili tumejipanga ili kufanikisha lengo la kushinda na kusonga mbele katika Michuano hii ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.”

Katika hatua nyingine Zola amekiri walifanya makosa makubwa katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza na kupoteza 1-0, lakini ameahidi kikosi chao kitapambana kufa na kupana leo Ijumaa, ili kutunza heshima katika Uwanja wao wa nyumbani.

“Tulifanya makosa ya kuruhusu bao lililowapa ushindi kule kwao lakini hapa watapoteza kwa kuwa tunataka kulinda heshima yetu hapa nyumbani hatujapoteza dhidi ya timu yoyote msimu huu.”

Arsene Zola Kiaku

“Nafikiri zitakuwa dakika tisini ngumu kwao lakini kwetu tutakuwa na presha ya kawaida kuwahamasishwa kushinda mapema kwa mashabiki wet, tunajua ubora wa Simba tunajua wanamtegemea sana Baleke hapa tutamdhibiti pamoja na wenzake.” Amesema Zola

Ili ifuzu Nusu Fainali Wydad AC italazimika kusaka ushindi wa mabao 2-0 ama zaidi katika mchezo wa leo, lakini Simba SC inahitaji sare ya aina yoyote ama ushindi ili kujihakikishia safari ya kucheza hatua inayofuata.

Azam FC yaanza kuivutia kasi Simba SC
Serikali yahimiza utoaji taarifa matukio ukatili wa kijinsia