Benchi la Ufundi la timu ya taifa, Taifa Stars, limeeleza kuwa tayari limeshaanza maandalizi ya kuelekea Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2023), zinazotarajiwa kuanza kunguruma Januari, mwakani nchini Ivory Coast.
Kocha Msaidizi wa Stars, Hemed Morocco amesema kuwa walishaanza kujipanga kuhusiana na michuano hiyo siku moja baada ya kufanikiwa kufuzu kutokana na matokeo ya suluhu dhidi ya Algeria na hivyo kumaliza nafasi ya pili Kundi F ikiwa na pointi nane dhidi ya Uganda yenye saba na Niger yenye mbili.
Amesema wao kama benchi wameanza mikakati wakiwa na dhamira ya kukisuka kikosi cha ushindani pamoja na programu sahihi za kuhakikisha wanakwenda kufanya vizuri katika michuano hiyo.
“Baada ya kupata nafasi tu, tulikaa na kujadili cha kufanya, tumejua tuna kazi ya kufanya na tumeanza maandalizi tayari, tunaangalia programu za kufanya katika maandalizi ingawà mipango yetu inasubiri muunganiko wa taasisi nyingine ili tujue tunaanza vipi au tuna changamoto ipi,” amesema Morocco.
Pia, kocha huyo amefafanua kuwa wamebaini yapo mengi ya kurekebisha ndani ya kikosi ili angalau kupata kitu bora ambacho kitawafurahisha watanzania kwa ujumla.
Ameeleza kuwa wanahitaji sapoti ya watanzania wote kuelekea michuano hiyo ndio maana wanasuka mipango madhubuti na kuhakikisha wanafanya vizuri kuliko michuano mingine iliyopita waliyowahi kushiriki.
Hii ní mara ya tatu Tanzania inashiriki michuano hiyo ya 34 sasa ambayo bingwa mtetezi ni Senegal baada ya kushiriki mwaka 1980 nchini Nigeria kisha mwaka 2019 nchini Misri na kuishia hatua ya makundi.