Kocha Mkuu wa Simba SC, Abdelhak Benchikha amerejesha matuamini kwa Mashabiki na Wanachama wa timu hiyo na amekabidhiwa faili la Jwaneng Galaxy ya Botswana ambao watakutana nao kesho Jumamosi (Desemba 02) katika mchezo wa Mzunguuko wa Pili wa Kundi B, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Kocha huyo kutoka nchini Algeria amesema kazi kubwa ni kufanyia kazi mechi iliyopo mbele yao kwa kusahihisha makosa yao lakini pia kufanyia kazi ubora wa wapinzani wao ambao wamewaona katika michezo iliyopita.
Amesema amekutana na walimu walikuwa na jukumu la kuongoza timu hiyo kipindi bado hajapewa jukumu la kukinoa kikosi hicho kwa kuwaeleza walipoanzia na walipofikia na kukabidhiwa masuala yote na kuendelea alipoishia ili kwenda kusaka matokeo chanya ugenini.
“Nimewakumbusha wachezaji majukumu yao na kuhakikisha wanajituma ili kuwapa furaha Mashabiki na Wanachama, ninaamini kwa pamoja tunaweza kubadili hali ya hewa iliyopo sasa na kurudisha furaha na kuanza kupata ushindi.
“Ni kweli kuna mechi mbele yetu kazi tumeanza kuifanya, wachezaji wanaelewa nini wafanye tunahitaji kushinda hiyo mechi, kila mmoja anatakiwa kujituma kwa ajili ya timu na kutumikia nembo ya klabu,” amesema kocha huyo.
Amesisitiza kuwa kuhitaji mchezaji ambaye anajituma na kufanya majukumu yake na hatakuwa tayari kumvumilia mchezaji yoyote ambaye atakwamisha majukumu yake.
Tayari Kikosi cha Simba SC kimeshawasili nchini Botswana kwa ajili ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy, huku Aishi Manula, John Bocco na Shaban Iddy Chilunda wakiachwa jijini Dar es salaam.
Aishi ameachwa kwa sababu aliumia akiwa kwenye majukumu ya timu ya taifa wiki iliyopita, lakini Bocco na Chilunda hawapo kwenye mpango wa Benchika katika mechi yake ya kwanza kazini Simba SC.
Ikumbukwe mechi ya kwanza ya Kundi B Ligi ya Mabingwa, Simba ililazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na ASEC Mimosas ya Ivory Coast Uwanja wa Benjamín Mkapa Jijini Dar es Salaam Jumamosi iliyopita.