Wakati Simba SC ikitarajia kukutana na Wydad Casablanca Jumamosi (Desemba 09), Kocha Mkuu Abdelhak Benchikha amefichua udhaifu aliokutana nao tangu alipoanza kazi klabuni hapo.
Benchikha alianza rasmi kazi Simba SC juma lililopita, ikiwa ni siku chache kabla ya mchezo wa Mzunguuko wa Pili wa Kundi B, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana, uliomalizika kwa sare ya 0-0.
Kocha huyo kutoka nchini Algeria amesema baada ya kufanya kazi kwa siku kadhaa, amebaini wachezaji wake hawana utimamu wa mwili, hali ambayo imekuwa kikwazo cha utendaji mzuri wa kazi Uwanjani.
Banchikha amesema kazi kubwa alinayo, pamoja na kuitengeneza timu yake kuifundi kwa ajili ya kukabiliana na Wydad Casablanca, lakini pia ni kupandisha kiwango cha utimamu wa mwili ambacho kilikuwa chini mno.
“Wachezaji hawakuwa na utimamu wa mwili, yaani ilikuwa chini ya kiwango na ndiyo eneo ambalo nimewekeza nguvu kweli kweli, kiufundi Simba SC ina wachezaji wazuri sana, levo ya utimamu wa mwili ndiyo inawasumbua, na nimemwachia kazi mwalimu mwenzangu Kamal Boujdjenane anaifanya kazi hiyo,” amesema kocha huyo aliyechukua nafasi ya Roberto Oliveira.
Amesema anadhani ndiyo sababu inaonekana kama baadhi ya wachezaji wameshuka viwango, au wana Umri mkubwa unaowafanya washindwe kukabiliana na mikiki mikiki.
“Nadhani ndiyo ilionekana kama wachezaji wanaonekana kama viwango vyao vimefikia ukingoni, lakini kwa sasa inaanza kuongezeka na itaongezeka zaidi, kwa sasa tunahitaji angalau asilimia 50 tu ya ufiti wa wachezaji iweze kuwa kwenye ushindani unaotakiwa,” amesisitiza kocha huyo.