Kauli ya Kocha Mkuu wa Simba SC Abdelhak Benchikha ya kutoa nafasi kwa kila mchezaji na yule atakayemshawishi, basi ataingia moja kwa moja kikosi cha kwanza, ni dhahir inakwenda kuvunja kikosi kilichoachwa na Kocha aliyemtangulia Roberto Oliveira ‘Robertinho’.
Benchikha alitoa kauli hiyo juzi Jumanne (Novemba 28) alipozungumza na Waandishi wa Habari kwa mara ya kwanza tungu alipowasili jijini Dar es salaam Jumatatu (Novemba 27).
Kocha huyo kutoka nchini Algeria tayari ameanza jukumu la kukinoa kikosi hicho, ambacho kinajiandaa na mchezo wa Mzunguuko wa Pili wa Kundi B, Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy ya nchini Botswana.
Benchikha alisema ana imani na wachezaji wote aliowakuta, kikubwa anataka kuona kila mchezaji akipambania wakati akiendelea kukisuka kikosi hicho.
Aliongeza kuwa atatumia kipindi hiki kutengeneza kikosi sambamba na kuangalia sehemu zenye upungufu kwa ajili ya kuboresha katika dirisha dogo, kwa kuingiza maingizo mapya.
“Nimepanga kutoa nafasi kwa kila mchezaji, atakayeonesha kiwango bora atanifaa. Kikubwa ninataka kuona kila mchezaji anatumia vema nafasi atakayoipata kuhakikisha anapambana kuipa matokeo mazuri timu.
“Ninataka kuona ninarejesha matumaini ya mashabiki katika timu yao, baada ya kuanza kazi ya kuifundisha Simba SC ambayo ninaamini tutafikia malengo yetu ya msimu huu,” alisema.