Kocha Mkuu wa Simba SC, Abdelhak Benchikha amefichua kuwa mpango wake wa kwanza mkubwa ni kuhakikisha anapata matokeo katika mchezo wake wa kwanza hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana.
Benchikha ametoa kauli hiyo ikiwa tayari kikosi chake kimewasili salama nchini Bostwana kwa ajili ya mchezo huo utakaopigwa kesho Jumamosi (Desemba 02).
Kocha huyo kutoka nchini Algeria amesema kuwa kazi kubwa ni kufanyia kazi mchezo uliopo mbele yao kwa kusahihisha makosa lakini pia kufanyia kazi ubora wa wapinzani wao ambao wamewaona katika michezo yao.
Amesema kuwa amekutana na makocha ambao walikuwa na jukumu la kuongoza timu hiyo kipindi bado hajapewa jukumu la kukinoa kikosi hicho kwa kuwaeleza walipoanzia na walipofikia na kukabidhiwa masuala yote na kuendelea alipoishia ili kwenda kusaka matokeo chanya ugenini.
“Nimewakumbusha wachezaji majukumu yao na kuhakikisha wanajituma ili kuwapa furaha mashabiki, ninawaamini kwa pamoja tunaweza kubadili hali ya hewa iliyopo sasa na kurudisha furaha na kuanza kupata ushindi.
“Ni kweli kuna mechi mbele yetu kazi tumeanza kuifanya, wachezaji wanaelewa nini wafanye tunahitaji kushinda hiyo mechi, kila mmoja anatakiwa kujituma kwa ajili ya timu na kutumikia nembo ya klabu” amesema Benchikha
Aidha amesisitiza kuwa anahitaji kuona kila mchezaji anajituma na kufanya majukumu yake na hatakuwa tayari kumvumilia mchezaji yeyote ambaye atakwamisha majukumu yake.
Benchikha amesema anatambua ugumu michuano ya Ligi ya Mabingwa lakini anaimani wachezaji wakiamua kujitoa na kupambania klabu watafanikiwa katika malengo yao ya kutwaa mataji na kuvuka Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.