Kocha Mkuu wa Simba SC Abdelhak Benchikha amekiri kutokufurahishwa na Washambuliaji wa timu yake, kufuatia kushindwa kuzitumia vyema nafasi walizozitengeneza katika michezo miwili iliyopita ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Benchikha amekiri kukabiliwa na changamoto hiyo, huku kikosi chake kikiwa katika maandalizi ya mwisho ya kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar utakaopigwa kesho Ijumaa (Desemba 15) katika Uwanja wa Uhuru, Dar es salaam kabla ya kuikaribisha Wydad Casablanca ya Morocco kwa Mkapa ikiwa ni mchezo wa marudiano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Katika mechi mbili zilizopita ambazo Benchikha ameiongoza Simba SC, timu hiyo ilishindwa kufunga bao ikilazimishwa suluhu na Jwaneng Galaxy ya Botswana kisha kulala l-0 mbele ya Wydad, huku nyota wa timu hiyo kama Kibu Denis, Jean Baleke, Moses Phiri, Saido Ntibazonkiza, Luis Miquissone na Willy Onana wakipoteza nafasi kadhaa za wazi.
Kutokana na hilo Benchikha amesema hajafurahishwa na kiwango cha washambuliji hao kwa walichoonyesha tangu atue kikosini jambo lililomfanya kufikiria kusajili mshambuliaji mpya anayejua kutumia vyema nafasi.
Kocha huyo kutoka Algeria, amesema licha ya kutengeneza nafasi nyingi katika mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika alizoiongoza Simba SC, washambuliaji wamemuangusha kwa kushindwa kufunga jambo ambalo sio zuri kwa timu.
“Tunatengeneza nafasi lakini tunashindwa kuweka mpira nyavuni. Hatuwezi kwenda hivyo. Washambuliaji wanapaswa kujitafakari katika mechi mbili zijazo kabla hatujaangalia namna nyingine ya kutibu tatizo hilo,” amesema Benchikha.
Baleke ndiye ametumika kama mshambuliaji wa kati katika mechi mbili zilizopita dhidi ya Jwaneng Gallaxy na Wydad Casablanca wakati washambuliaji wenza wakiwa ni Saidi Ntibanzokiza ‘Saido’, Kibu Denis, Willy Onana, Moses Phiri na Luis Miquissone waliotumika katika nyakati tofauti, lakini wameshindwa kufunga bao hata moja na kufanya Simba SC icheze dakika 180 bila bao.
Pamoja na hilo, Benchikha amesema timu inaendelea vizuri na kwa kushirikiana na benchi lake la ufundi wanatengeneza kikosi kitakachokuwa na ushindani na kufikia malengo.
Timu ina maendeleo mazuri, wachezaji wanajitoa na kufuata maelekezo kwa kiasi kikubwa, tunafanya kazi kwa umoja nia ikiwa ni kutimiza malengo tuliyojiwekea,” amesema Benchikha anayependelea soka la kasi.
Licha ya Benchikha kutoweka wazi mipango yake ya usajili, mmoja wa vigogo wa Simba SC, amefichuwa kuwa kocha huyo amewaambia viongozi anahitaji mchezaji mpya kwenye eneo la ushambuliaji na tayari amewapa jina la anayemtaka.
“Huyu kocha atafanya mabadiliko makubwa. Kwanza ametuambia tuanze mazungunmzo na mshambuliaji mmoja na jina lake ametupa lakini pia baada ya mechi mbili zijazo atatoa ripoti kamili itakayoeleza mahitaji yake kwa kina,” kimesema chanzo hicho.