Kocha Mkuu wa Simba SC Abdelhak Benchikha kwa mara ya kwanza amezungumza na Waandishi wa Habari na kueleza mipango na mikakati yake, baada ya kuwasili nchini usiku wa kuamkia leo.

Kocha Benchikha ambaye alikuwa huru kabla ya kusaini mkataba na Simba SC, amesema amefurahia kuwa sehemu ya klabu hiyo ya Msimbazi, na anatarajia mengi kutoka kwa Mashabiki, Wanachama, Viongozi pamoja na Wachezaji wake.

Amesema kabla ya kuwasili Tanzania alikuwa anaifuatilia Simba SC, hivyo anafahamu kila kitu kilichokuwa kikiendelea klabuni hapo, na hana budi kusisitiza kuwa, amekuja kufanya kazi ya kuirudisha klabu hiyo kwenye mpango wa ushindi.

“Nina furaha kubwa kuwepo hapa. Tangu nilipoanza kuwasiliana na viongozi nilikuwa na shauku ya kuja. Jambo kubwa ambalo naomba ni mashabiki kutupa ushirikiano na naamini kupitia hilo tutafanikiwa pamoja.”

“Kuna mambo mengi ambayo tayari nayajua na nimekuja na mikakati ambayo taifanyia kazi. Kuhusu wachezaji tajua zaidi nikishaanza kazi, kuhusu mashindano ya ndani na kimataifa yote ni muhimu. Mimi ni mpambanaji na nitapambana hadi tutafika.” amesema kocha huyo kutoka nchini Algeria

Katika hatua nyingine Kocha huyo aliyetwaa Ubingwa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kuifunga Young Africans na kisha Ubingwa wa CAF Super Cup kwa kuifunga Al Ahly ya Misri, ametoa wito kwa Mashabiki na Wanachama kumpa ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha mipango ya mafanikio.

“Mafanikio yatajengwa na Wanasimba wote hilo ndio muhimu zaidi. Kwa wachezaji sitaangalia majina bali anayefanya vizuri, kiwango cha mchezaji ndio kitafanya nimtumie.” amesema

Kocha Benchikha anatarajiwa kuanza kazi ya kukiandaa kikosi chake tayari kwa mchezo wa Mzunguuko wa Pili wa Kundi B, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy utakaopigwa Botswana Jumamosi (Desemba 02).

CEO Simba SC afichua walivyompata Benchikha
Wakwamishaji changamoto za Walimu kukiona