Kocha Mkuu wa Simba SC Abdelhak Benchikiha amesema anawafahamu vizuri wapinzani wake Wydad Casablanca, ambao watakuwa nyumbani mjini Marrakesh-Morroco kwa ajili ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Mchezo huo wa Mzunguuko watatu wa Kundi B, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, utapigwa kesho Jumamosi (Desemba 09) mishale ya saa nne usiku kwa saa za Afrika Mashariki, huku kila timu ikihitaji ushindi ili kujisafishia njia ya kuisaka Robo Fainali ya michuano hiyo mikubwa Barani Afrika upande wa Vilabu.
Benchikha amekiri kuifahamu vyema Wydad Casablanca akiwa katika Mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika leo Ijumaa (Desemba 08) majira ya mchana mjini Marrakesh-Morocco.
Kocha huyo ambaye amewahi kuvinoa baadhi ya vilabu vya soka nchini Morocco amesema Wydad Casablanca ina kikosi chenye ubora na kinachofahamu nini maana ya kupambana ndani ya Uwanja, hivyo anatarajia upinzani mkubwa kutoka kwao katika mchezo wa kesho.
Benchikha amesema pamoja na kutambua hivyo, bado kikosi chake cha Simba SC kinabebwa na sifa kama hizo za wapinzani wake, na ana uhakika kitaingia Uwanjani kwa lengo la kwenda kusaka alama tatu muhimu ambazo zitakuwa na faida kubwa sana kwa upande wao.
“Ni mchezo mwingine ngumu tuliokuja kucheza ugenini, huku tukiwa na lengo kubwa la kupata alama tatu, nawafahamu vizuri wapinzani si mara ya kwanza kukutana nao wana timu nzuri, ila naamini tutakuwa bora dhidi yao” amesema Abdelhak Benchikiha
Timu hizo zinakwenda kukutana kwenye mpamnbano huo zikiwa hazijashinda michezo miwili iliyopita, ambapo upande wa wenyeji Wydad Casablanca walikubali kupoteza 1-0 dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana na Asec Mimosas ya Ivory Coast.
Simba SC iliambulia matokeo ya sare ya 1-1 dhidi ya Asec Mimosas katika mchezo wa Mzunguuko wa kwanza uliopigwa jijini Dar es salaam, huku ikiambulia sare ya bila kufungana dhidi ya Jwaneng Galaxy ugenini nchini Botswana.