Kocha Mkuu wa Simba SC, Abdelhak Benchikha, amekiri kuwa kikosi chake kinazidi kuimarika ila kuna tatizo moja la ufungaji ambalo ameahidi kulifanyia kazi, akisifu kiwango cha wachezaji wake, lakini akilia na mwamuzi aliyechezesha mechi ya Mzunguuko watatu wa Kundi B, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Wydad Casablanca, akisema aliongeza dakika tatu zaidi kitu ambacho si cha kawaida.

Benchikha amesema mechi dhidi ya Wydad Casablanca ilikuwa nzuri ingawa ilikuwa na baadhi ya changamoto zilizosababisha wakose matokeo mazuri.

“Tulicheza vizuri, tuliwafanyia Wydad pressing hadi dakika ya 90, tukafungwa goli dakika za mwisho ambalo ni kama tulikosa umakini hadi mwisho wa mchezo.

“Ninachofurahia kwenye timu yangu ni kuweza kuzuia na kushambulia kwa kasi, eneo la kuweka mpira nyavuni ndilo tumeshindwa kufanikisha, nadhani kuna haja ya kukaa na kulifanyia kazi, lakini nimeridhishwa na timu ilivyocheza,” amesema kocha huyo raia wa Algeria ambaye hana muda mrefu tangu aitwae timu hiyo kutoka kwa Mbrazili Robertinho.

Amesema kwa sasa wamerejea nyumbani kujiandaa na mechi ya marudiano ambayo atataka kujipanga vizuri kuhakikisha Simba SC inaibuka na ushindi.

“Mechi ya marudiano tutajipanga vizuri na kuhakikisha tunakuwa sahihi zaidi ili nasisi tushinde kwa kuwa tutakuwa nyumbani kama ilivyokuwa kwao, ameongea kocha huyo.

Benchikha amelalamikia kitendo cha mwamuzi wa mechi hiyo kuongeza dakika tatu baada ya tatu za majeruhi kumalizika.

“Aliongeza dakika tatu tukacheza hadi dakika ya 96, si kitu cha kawaida sijui kwa nini alifanya hivyo, lakini ndio hivyo,” alilalamika Benchikha.

Naye Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, hakusita kumpa sifa kocha huyo akisema ni mwanamapinduzi aliyefanya mapinduzi makubwa ndani ya kikosi hicho kwa muda mfupi tu.

“Ndani ya muda mfupi amefanya mapinduzi makubwa ndani ya kikosi chetu, utimamu wa mwili kwa wachezaji umepanda maradufu, ukabaji wa hali ya juu, ufundi umeongezeka kwa baadhi ya wachezaji wetu, kiwango cha mchezaji mmoja mmoja kimepanda, hali ya kujiamini imeongezeka na morali iko juu,” amesema.

Simba SC imerejea nchini jana Jumatatu (Desemba 11) na wachezaji kupewa mapumziko ya siku moja kabla ya leo Jumanne (Desemba 12) kuanza mazoezi kwa ajili ya mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar na kisha Jumanne ijayo kuikaribisha Wydad Casablanca katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwenye mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Tanzia, Director Nisher afariki Dunia
Young Africans yampambania Ranga Chivaviro