Nahodha na Beki Mkongwe wa Maafande wa Jeshi la Magereza ‘Tanzania Prisons’ Benjamin Asukile amesema kikosi chao kipo tayari kwa mchezo wa leo Jumatatu (Mei 09) dhidi ya Young Africans.
Tanzania Prisons ambayo msimu huu imekua na matokeo mabaya, itakua mgeni wa Young Africans Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza kwa 1-0 dhidi ya Mbeya Kwanza FC.
Asukile ambaye anasifika kwa kucheza kwa nguvu bila kuchoka ndani ya dakika 90, amesema wamejiandaa vyema na wanajua namna ya kuikabili Young Africans ili kupata matokeo yatakayowasaidia kujinasua mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu.
Amesema watapambana na Young Africans na kila mchezaji atakua na jukumu la kuiwezesha Tanzania Prisons kufikai lengo lake la kusaka alama tatu, na hawatokua na dhamira ya kumtazama mchezaji mmoja mmoja wa timu pinzani.
“Tuna mabeki wanajua kazi yao, ukimuongelea sana Mayele unakuwa unakosea wachezaji wapo wengi sana yeye ni mchezaji kama wachezaji wengine, ukimuongelea sana yeye haileti maana yoyote, kila mchezaji yupo uwanjani kutetea Timu yake,”
“Kupoteza mechi ya kwanza nyumbani wala siyo shida maana matokeo ya mpira ndivyo yalivyo, nafasi aliyopo Yanga na sisi kama wao wana kiu ya kupata ubingwa sisi tuna kiu ya kuondoka huku tulipo kwa hiyo nafikiri game itakua ya aina yake.” amesema Asukile
Klabu hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Magereza Tanzania, inashika nafasi ya 15 ikiwa na alama 22, huku Young Africans ikiwa kileleni kwa kuwa na alama 56.