Benjamin Mendy amerejea kwenye soka baada ya kupata timu ya kuichezea ikiwa ni wiki chache tangu alipoachana na Manchester City.
Beki huyo wa kushoto, mshindi wa Kombe la Dunia amesaini kujiunga na Lorient ya Ligue 1 hadi Juni 2025 ikiwa ni siku chache zimepita baada ya kukutwa hana hatia kwenye kesi ya ubakaji iliyokuwa ikimkabili.
Mendy aliachana na Man City kwa makubaliano ya pande mbili mwezi uliopita huku mkataba wake ukiwa umefika tamati na hajacheza mechi yoyote kwenye kikosi hicho cha mabingwa wa Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya tangu 2021.
Taarifa ya klabu yake mpya ilisomeka hivi: “FC Lorient ina furaha kutangaza kumsajili beki wa kushoto wa kimataifa wa Ufaransa, Benjamin Mendy (29).
Baada ya kufanyiwa vipimo vya afya Mendy, bingwa wa Kombe la Dunia 2018, mshindi wa mataji manne ya Ligi Kuu England akiwa na Manchester City na bingwa wa Ligue 1 akiwa na Monaco anakuja kuongeza nguvu Lorient.”
Mendy, alisafishwa juu ya kesi ya kubaka iliyokuwa ikimkabili.
Ijumaa iliyopita alisherehekea kuwa huru akiwa na marafiki zake ambapo walikuwa na mtoko maalumu. Mendy, alishutumiwa kumbaka mwanamke mwenye umri wa miaka 29 nyumbani kwa mchezaji huyo, Oktoba 2018.
Hakukutwa na hatia pia juu ya kesi hiyo ya kumbaka mwanamke mwenye umri wa miaka 24 katika tukio lililodaiwa kutokea kwenye makazi yake yenye thamani ya Pauni 4.8 milioni huko Prestbury, Cheshire.