Beki wa Mabingwa wa Soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich, Benjamin Pavard anadaiwa kulazimisha Usajili wake wa kujiunga na Manchester United katika dirisha hili baada ya klabu hiyo ya mjini Munich kukataa ofa ya kwanza ya Masheni Wekundu iliyowasilishwa siku chache zilizopita.

Pavard mwenye umri wa miaka 27, mkataba wake wa sasa na Bayern Munich unatarajiwa kumalizika mwakani na anataka kuondoka kwa ajili ya kutafuta changamoto mpya sehemu nyingine ikiwa ni baada ya kuhudumu kwenye Ligi Kuu ya Ujerumani kwa muda mrefu.

Msimu uliopita beki huyo wa upande wa kulia na mwenye uwezo wa kucheza katikati alicheza mechi 43 za michuano yote na beki wa Man United Raphael Varane ambaye ni Mfaransa mwenzake ndio anadaiwa kumshawishi sana staa huyu ajiunge nao.

Hadi sasa Man United imeshafikia makubaliano binafsi na beki huyo kwenye masuala ya mshahara na bonasi ya usajili na kinachosubiriwa ni kukubaliana na Bayern Munich kwenye masuala ya ada ya uhamisho ambayo ofa ya kwanza ndio hiyo imekataliwa.

Man United inahangaika kumsajili Pavard ili kuboresha eneo lao la ulinzi ambalo kwa msimu uliopita lilikuwa katika ubutu mkubwa, huku inatarajiwa kuachana na staa wake, Harry Maguire anayecheza nafasi sawa na Pavard.

Maguire yuko kwenye hatua ya mwisho kukamilisha uhamisho wake kwenda West Ham, ambapo dau la Pauni 30 milioni limeshakubaliwa.

Elimu bora: Wanafunzi wa kike wawezeshe - Dkt. Tulia
Pluijm: Ngao ya Jamii itatusaidia Kimataifa