Benki Mpya ya Serikali ya Biashara ya Tanzania (Tanzania Commercial Bank- TCB PLC) tawi la Shinyanga imeshiriki Maonesho ya Pili ya Biashara na Teknolojia ya Madini Mkoa wa Shinyanga ikiwa ni sehemu ya kutangaza muonekano wao mpya kutoka iliyokuwa Benki ya TPB na sasa Benki ya TCB.
Maonesho ya Pili ya Biashara na Teknolojia ya Madini Mkoa wa Shinyanga yanayoongozwa na kauli mbiu “Uwekezaji wa Madini na Viwanda Shinyanga kwa Uchumi Endelevu” yameanza tarehe 23 Julai, yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 1 Agosti, 2021 katika uwanja wa Zainab Telack kijiji cha Butulwa kata ya Old Shinyanga Manispaa ya Shinyanga.
Akizungumza kwenye maonesho hayo, Meneja wa Benki ya Biashara ya Tanzania (Tanzania Commercial Bank- TCB PLC), Tawi la Shinyanga Julius Mataso amesema wanashiriki maonesho hayo kama wadau wa biashara na taasisi ya fedha wezeshi ya biashara katika mkoa wa Shinyanga.
“Tumeshiriki maonesho haya kwa ajili ya kujitangaza muonekano wetu mpya kutoka iliyokuwa Benki ya TPB na kuwa Benki ya Biashara ya Tanzania (Tanzania Commercial Bank- TCB PLC”,amesema Mataso.
“Kufuatia mabadiliko haya tunapenda kuwataarifu wateja wetu na Watanzania kwa ujumla kuwa tumebadilisha muonekano wa Nembo na jina la Benki. Mabadiliko haya yanaenda sambamba na kuboresha huduma zetu ili kukidhi kiu ya Wateja wetu na Watanzania kwa ujumla na kwa kutoa huduma za viwango vya hali ya juu”,amesema Mataso.
“Miongoni mwa huduma tunazozitoa na tulizozifanya kuwa rafiki zaidi kwa wateja ni pamoja na huduma ya bima ya maisha ambapo kila mteja wetu aliye na akaunti kwenye benki ya TCB anakuwa na sifa ya kupata huduma ya bima ya maisha ambapo tunatoa mkono wa pole kwa mteja anapofiwa na mtegemezi (mme, mke au watoto wasiozidi umri wa miaka 18) au yeye mwenyewe anapofariki dunia. Hii faraja tunaitoa kwa kiasi cha shilingi milioni 2”,amesema.
Ameeleza kuwa ili kupata bima ya maisha kupitia Benki ya TCB hakuna haja ya kujaza fomu ya kujiunga kwani ukishakuwa tu akaunti ya TCB basi unakuwa tayari na sifa za kupata huduma hiyo.
Ameongeza kuwa bima hiyo ya maisha pia wanaitoa kwa wanachama walio ndani ya vikundi mbalimbali vilivyojiunga kwa ajili ya kusaidiana katika masuala ya kijamii.“Lakini pia katika Benki ya TCB tunatoa huduma za bima za mali kama vile magari, nyumba n.k”,amesema.
Aidha amewaomba Watanzania kuchangamkia huduma ya Akaunti ya Muda Maalumu ‘Fixed Depost Account’ inayotolewa katika Benki ya TCB ambayo wanatoa riba ya asilimia 11 kwa mwaka.
Amezitaja huduma zingine ni pamoja na huduma ya mikopo ya aina mbalimbali kama vile mikopo ya watumishi, wastaafu, wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa. Huduma zingine ni huduma ya kutuma na kupokea fedha ya Western Union.
“Tunawakaribisha Wana Shinyanga na Watanzania kwa ujumla kuja kupata huduma za kifedha katika benki yetu kwenye matawi yetu yaliyotapakaa nchi nzima. Tunawaahidi kuendelea kutoa huduma nzuri na bora”,amesema Mataso.