Benki ya Dunia imekubali kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na athari za mafuriko zinazosababishwa na mvua kubwa zinazonyesha kila mwaka katika jiji la Dar es salaam na kuleta madhara makubwa hasa katika maeneo ya mabondeni na hususani eneo la Jangwani.
Taarifa hiyo imesemwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango wakati akizungumza na wajumbe wa Benki ya Dunia walioongozwa na Bi Bella Bird ambaye ni Mkurugenzi wa Benki hiyo kwa nchi za Tanzania, Somalia, Burundi na Malawi katika mikutano ya kipupwe inayoendelea kufanyika mjini Washington DC.
Mvua zimekuwa janga kubwa jijini Dar es salaam kutokana na miundombinu inayoshindwa kukidhi athari zinazoletwa na mvua, mji umekosa mifereji imara yenye uwezo wa kusafirisha maji na kuyamwaga baharini, lakini pia bado madaraja hayana uwezo wa kuhimili mvua zinazonyesha nchini mengi yao kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha yamevunjika na kusababisha barabara kufungwa na ndio maana kipindi cha mvua kunakuwa na ongezeko kubwa la foleni barabarani.
Hivyo kwa kushirikiana na Benki ya Dunia serikali imeamua kulivalia njuga tatizo hilo ili kupunguza maafa yatokanayo na mvua hizo, kama ilivyo mwaka huu nchi imepoteza nguvu kazi baada ya kupoteza watu 12 waliofariki dunia kutokana na mvua kubwa zilizonyesha mfululizo wa siku tatu.