Hatimaye Benki ya Dunia imeridhia kuikopesha Serikali ya Tanzania kiasi cha $500 milioni kwa ajili ya kusaidia kuendeleza sekta ya elimu hasa kwa shule za sekondari, kiasi kilichokuwa kimezuiwa kwa muda kutokana na madai yaliyowasilishwa na wanasiasa na wanaharakati.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Benki ya Duania leo, Aprili 1, 2020 mkopo huo utawafaidisha zaidi ya wanafunzi wa sekondari milioni 6.5 nchini kwa kuimarisha uwezo wa Serikali katika kuboresha na kuimarisha mifumo ya elimu nchini.
“Kila mwanafunzi nchini Tanzania anastahili kupata elimu bora, lakini kila mwaka maelfu wanakosa fursa hii ya kubadili maisha yao; programu hii itasaidia kuwaweka vijana wadogo nchini humo mstari wa mbele.
Pia, imetenga theluthi mbili ya rasilimali zake kwa ajili ya kuboresha mazingira ya elimu kwa watoto wa kike,” Mkurugenzi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania, Bi. Mara Warwick amesema.
Aliongeza, “hii ni hatua muhimu katika kutatua changamoto zinazowakabili watoto nchini Tanzania katika sekta ya elimu. Benki ya Dunia tutaendelea na mazungumzo yetu na Serikali kwa upana kuhusu usawa katika utoaji elimu kwa watoto mashuleni.”
Mwaka jana, Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe na baadhi ya wanaharakati waliwasilisha malalamiko Benki ya Dunia wakiitaka kusitisha uamuzi wa kuikopesha Tanzania kiasi hicho cha fedha kwa madai kuwa mfumo wa elimu unawabagua watoto wa kike. Walijikita zaidi kupinga uamuzi wa Serikali kuzuia wasichana wanaopata ujauzito kuendelea na masomo kama kawaida.
Benki ya Dunia ilisimamisha mchakato wa utoaji mkopo huo, lakini baada ya ufuatiliaji na michakato mingine wamefikia uamuzi wa kuikopesha Serikali ya Tanzania.