Baada ya kupewa Mkono wa Kwaheri na Uongozi wa Simba SC, Mlinda Lango Beno Kakolanya amefunguka sababu zilizopeleka  kuachana na klabu hiyo ambayo ameitumikia kwa zaidi ya miaka mitatu mfululizo.

Kakolanya alithibishwa rasmi kuwa hatokuwa sehemu ya kikosi cha Wekundu hao wa Msimbazi jana Alhamis (Juni 23), na tayari ameshaanza kuhusishwa na mpango wa kujiunga na Singida Fountain Gate (Singida Big Stars).

Mlinda Lango huyo amesema sababu kubwa iliyopelekea kuondoka Simba SC ni kushindwana na Uongozi wa juu katika harakati za kusaini mkataba mpya, ambapo baadhi ya matakwa yake hayakufikiwa.

“Viongozi wa Simba walinipa ofa ambayo sikukubaliana nayo na nikawaomba waniongezee kidogo lakini waligoma nikaamua kuchukua maamuzi ya kutafuta maslahi sehemu nyingine hasa ukichukulia mpira ndio kazi yangu na umri unakwenda,” amesema Kakolanya

Aidha, Mlinda Lango huyo amesema sababu ya timu hiyo kushindwa kufanya vizuri msimu uliopita ni baadhi ya wachezaji kupoteza ari ya kujituma kitu ambacho kiliwaangusha na kukosa matokeo mazuri katika baadhi ya mechi.

Amesema hata kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa lengo lao lilikuwa ni kufika angalau Nusu Fainali lakini ilishindikana kutokana na kutokuwepo kwa moyo wa kupambania timu.

Kakolanya ameitumikia Simba kwa misimu mitatu mfululizo na katika kipindi chote hicho ameweza kubeba mataji mawili ya Ligi Kuu, Ngao ya Jamii mbili na kuifikisha timu hiyo hatua ya Robo Fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Ifahamu nchi ndogo zaidi duniani
Chalamila kushuhudia masumbwi Mlimani City