Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana Bernard Morrison ameshindwa kutekeleza maagizo ya Uongozi wa Simba SC ya kutakiwa kuandika Barua ya kujieleza kufuatia tuhuna za utovu wa nidhamu.
Morrison alisimamishwa Simba SC juma lililopita kwa sababu za utovu wa nidhamu ambao haukuwekwa wazi kwenye taarifa iliyosambazwa kwenye vyanzo vya habari vya klabu hiyo kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Taarifa kutoka kwa watu wa karibu wa Morrison wamesema mchezaji huyo hajaandika na wala hajawasilisha maelezo kwenda kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba SC Barbara Gonzalez.
Watu hao wamedai kuwa Morrison amesisitiza hana kosa na hawezi kuandika maelezo yoyote, huku wazee wa klabu ya Simba SC wakiutaka uongozi wa klabu hiyo kuachana na Morrison haraka iwezekanavyo.
Aidha, Klabu ya Simba imethibitisha kutopokea barua ya maelezo kutoka kwa Morrison ambaye wamemsimamisha kwa makosa ya utovu wa nidhamu, Februari 4, 2022 ambapo klabu ya Simba ilitoa taarifa ya kumsimamisha mchezaji huyo.
Kwa mujibu wa Meneja wa Habari na Mawasilino wa klabu hiyo, Ahmed Ally amesema klabu bado haijapokea maelezo kutoka kwa mchezaji wao Bernard Morrison.