Baada ya kurejea Dar es salaam-Tanzania na kudaiwa amesaini Young Africans kwa mkataba wa miaka miwili, Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana Bernard Morrison, amefunguka Maisha yake ndani ya Klabu ya Simba SC ambayo bado ana mkataba nayo.
Morrison alilazimika kurejea nchini kwao Ghana baada ya kupewa mapumziko na Uongozi wa Simba SC hadi mwishoni mwa msimu huu, alirejea Dar es salaam juzi Jumanne (Juni 27) na kufanya mahojiano na Global TV.
Katika mahojiano hayo, Morrison amesema mambo kadhaa ambayo anaamini hayakuwa sawa akiwa ndani ya kikosi cha Simba SC na baada ya kupewa ruhusa ya mapumziko.
Morrison amesema: “Walinipa mapumziko maana nilikataa kusaini mkataba mpya, kama ningecheza Simba miaka 5 au 10 alafu mwisho wa siku nikarudi Ghana sina hela au kumpigia mwenyekiti naomba hela kuisaidia familia yangu sio kitu kizuri”
“Niliomba mkataba mzuri, maboresho kwenye mkataba ili niwe vizuri kuihudumia klabu na haikufanyika hivyo, nilikuwa na kikao na Barbara na sababu ya hicho kikao ni kwa sababu tulicheza mechi dhidi ya Yanga na ile mechi nilipata majeraha na awali tayari nilikuwa majeruhi kwenye mechi dhidi ya Orlando Pirates”
“Baada ya mechi daktari hakunifuata kunihudumia wala kujua hali yangu, nilimtumia meseji nyingi kuwa sipo sawa lakini hakufanya hivyo, niliwaambia hamnijali hivyo nililazimika kujihudumia mwenyewe nikiwa nyumbani”
“CEO alinipigia simu nikaenda ofisini kwake akaniambia wachezaji wanahasira, wanasema hawataki niende tena kambini wala mazoezini, kocha analalamika siwaheshimu, hawataki niende mazoezini hivyo malalamiko ni mengi ni kwa nini nafanya hivyo?”
“Nilimjibu sio kweli sidhani kama wachezaji wanaweza kufanya hivyo maana ndio hao hao wachezaji wananipigia simu nisipoonekana kambini kunijulia hali lakini wewe CEO unasema hivi, Bocco, Mkude, Chama, Bwalya walikuwa wananijulia hali kila siku,”