Hatimaye Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC umekubali kumsamehe Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana Bernard Morrison na kumrudisha kambini.
Morrison alisisamishwa klabuni hapo majuma mawili yaliopita, kwa utovu wa nidhamu wa kutoroka kambini, hali iliyopelekea kiungo huyo kuukosa mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast.
Maamuzi ya kusamehewa na kurudishwa kambini, yamefikiwa na Uongozi wa Simba SC baada ya Morrison kuomba radhi kwa njia ya maandishi kwa Uongozi na wachezaji wa klabu hiyo.
“Amefika ofisini kwa mtendaji mkuu wa klabu na walikuwa na mazungumzo ikiwemo pia mchezaji huyo kuomba radhi mbele ya CEO na kuahidi kutorudia makosa yake hayo na ameeleza pia kujutia hayo makosa yake.”
“Klabu imefikia maamuzi hayo kwa maslahi ya pande zote mbili yani mchezaji pamoja na timu” Imeeleza taarifa ya Simba SC kupitia Simba APP
Rasmi Kiungo huyo ameanza mazoezi na wenzake kuelekea mchezo wa Kombe la Shirikisho Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting utakaopigwa kesho Jumatano (Februari 16), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.