Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana na Klabu ya Simba SC Bernard Morrison amewataka Mashabiki wa klabu hiyo kuamini timu yao bado ina nafasi kubwa ya kutinga hatua ya Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Morrison ametoa nasaha hizo kwa Mashabiki wa Simba SC, akiwa mjini Benin ambako jana Jumapili (Machi 20) walikubali kupoteza mchezo wa Mzunguuko watano wa ‘Kundi D’ dhidi ya ASEC Mimosas kwa mabao 3-0.
Kiungo huyo mwenye sifa ya vituko na ucheshi amesema kupoteza kwa Simba SC katika mchezo huo sio mwisho wa safari ya matumaini ya kutinga hatua ya Robo Fainali ya michuano hiyo ya Barani Afrika, hivyo amewataka Mashabiki na kila mtu anayehusika na klabu hiyo kuendelea kuwa na matumaini kuelekea mchezo wa mwisho dhidi ya USGN.
“Tumepoteza hapa lakini hatujatolewa, tunaamini na tunajiamini kwamba kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya US Gendarmerie utakuwa mchezo wetu wa kufuzu kwa hiyo kila mmoja lazima awe imara.” Amesema Bernard Morrison ambaye aliingia kipindi cha pili katika mchezo dhidi ya ASEC Mimosas jana Jumapili (Machi 20).
Katika Msimamo wa ‘Kundi D’ Simba SC imeporomoka kutoka nafasi ya kwanza hadi ya tatu ikiwa na alama 07 sawa na RS Berkane ya Morocco inayoshika nafasi ya pili, huku ASEC Mimosas ikiongoza kwa kufikisha alama 09.
USGN inaendelea kuburuza mkia wa kundi hilo kwa kufikisha alama 05, baada ya kulazimishwa sare ya 2-2 dhidi ya RS Berkane jana Jumapili (Machi 20), ikiwa nyumbani Niger.
Michezo ya mwisho ya ‘Kundi D’ itachezwa April 03, ambapo Simba SC itakua nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kucheza dhidi ya USGN, huku ASEC Mimosas ikisafiri kulekea mjini Berkane-Morocco kupambana na wenyeji RS Berkane.
Mshindi wa kwanza na wapili katika kundi hilo watatinga hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu 2021/22.