Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana Bernard Morrison amekiri yeye ni shabiki namba moja wa winga mpya wa Young Africans, Mahlatse Makudubela ‘Skudu’ na anasubiri kwa hamu kuona nyota huyo atakavyowaonesha Watanzania vitu vya mpira ambavyo hata yeye alifundishwa na winga huyo.

Skudu aliyesajiliwa na Young Africans kutoka Marumo Gallants amewahi kucheza na Morrison wakiwa Orlando Pirates, lakini pia wakishabihiana aina ya uchezaji, wote wakitumika kama washambuliaji wa pembeni wakiwa na chenga za maudhi na mbwembwe nyingi.

Morrison aliyetemwa na Young Africans mwishoni mwa msimu uliopita 2022/233, ameeleza kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii kwamba, anajivunia kuhusika kumleta Skudu katika timu hiyo bila kufafanua namna alivyohusika.

“Namna furaha inavyoonekana, sihitaji kuzungumza sana kwa sasa. Nitazungumza baadae jinsi gani ninajivunia kukuleta hapa, nenda kaioneshe Tanzania vyote ulivyowahi kunifundisha. Mimi shabiki yako namba moja, nakupenda kijana wangu,” aliandika Morrison.

Morrison kuonesha kuwa amevutiwa mno na Skudu kutua Young Africans, aliibuka kwenye mazoezi ya kwanza ya mchezaji huyo na Young Africans akiwa amevalia jezi namba sita yenye jina Skudu akimkumbatia na kufurahi kwa kumuona.

Young Africans iliachana na Morrison baada ya kumalizika kwa msimu wa 2022-23 na sasa duru mbalimbali za michezo zinafafanua kuwa raia huyo wa Ghana anatarajia kutambulishwa na Singida Fountain Gate.

Rasmi Luis Miquissone arejea Simba SC
Gwiji Msimbazi aitabiria makubwa Simba SC