Uongozi wa klabu ya Coastal Union umekiri kushindwa kumpata Kocha kutoka nchini Kenya Bernard Mwalala ili kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Melis Medo aliyeondoka klabuni hapo majuma matatu yaliopita.
Mwalala ambaye aliwahi kuichezea Coastal Union pamoja na Young Africans kwa nyakati tofauti, alipendekezwa na Uongozi wa klabu hiyo ya jijini Tanga kufuatia uwezo wake na uzoefu alionao katika soka la Bongo, huku akikiongoza kikosi cha Kakamega Homeboyz kinachoongoza msimamo wa Ligi Kuu ya Kenya kwa sasa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Hamasa Coastal Union, Salim Bawazir, amesema mchakato wa kumnasa Kocha huyo umekwama na sasa wanaangalia mpango wa kumnasa kocha mwingine.
“Ni kweli tulikuwa na mpango wa kumchukua Ben Mwalala kuwa kocha mkuu wa Coastal Union, ili asaidiane na Joseph Lazaro, na yeye alikubali lakini imeshindikana kutokana na uongozi wa timu yake anayofundisha kugoma kuvunja naye mkataba, hivyo tumekwama hapo.
“Lakini baada ya kugonga mwamba tukamfikiria Mecky Mexime, lakini naye imeshindikana kutokana na kufundisha Kituo cha Akademi, hivyo Kamati ya Utendaji, Kamati ya Usajili na Kamati ya Mashindano bado zinaendelea na juhudi za kumtafuta kocha mkuu iwe ndani au nje ya nchi,” amesema Bawazir
Mwalala ambaye aliwahi kuwa kocha msaidizi wa Coastal Union kabla ya kushuka daraja na baadaye kurudi tena Ligi Kuu msimu wa 2017/2018, hadi sasa timu yake ya Kakamega Homeboyz inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Kenya inayoshirikisha timu 18, ikiwa na pointi 49 kileleni baada ya kushuka dimbani mara 23.
Kwa sasa kikosi cha Caostal Union kinaongozwa na Kocha Msaidizi Joseph Lazaro, huku klabu hiyo ikiwa nafasi ya 10 katika msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha alama 21, baada ya kushuka dimbani mara 18.