Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ureno na Klabu ya Manchester City, Bernardo Silva anasakwa na timu ya Saudi Arabia ya Al Hilal.
Mkataba wa Silva na Man City unatarajia kumalizika mwaka 2025 na klabu hiyo iko mbioni kumuongezea mkataba mwingine, huku akiwa na ofa kibao mezani.
Mabingwa wa Soka nchini Ufaransa Paris St-Germain (PSG) nao pia wanamtaka mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28, wakati Barcelona imekuwa ikihusishwa na Mreno huyo kwa miaka miwili iliyopita.
Hata hivyo, klabu zote zinaweza kufunikwa na mshahara mnono utakaoupata Silva endapo atakubali kutuwa Al Hilal ya Saudi Arabia.
Timu ya Al Hilal yenye maskani yake Riyadh, ambayo iko katika mchakato wa kumsajili, Ruben Neves kutoka Wolves, imekuwa ikifanya kila jitihada kutaka kumsajili Silva.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ureno amehusika katika mafanikio ya Man City kutwaa taji la Ligi Kuu chini ya Kocha Pep Guardiola baada ya kujiunga na klabu hiyo mwaka 2017.
Aliisaidia klabu hiyo kutwaa mataji matatu msimu huu, likiwemo lile la Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, Ligi Kuu na Kombe la FA.
Tayari wachezaji kibao wenye majina makubwa wameshatua katika klabu za Saudi Arabia. Mshambuliaji wa kimataifa wa Ureno, Cristiano Ronaldo alijiunga na Al Nassr Januari.
Kiungo Mfaransa, N’Golo Kante naye pia amekubali kujiunga na mabingwa wa ligi ya nchi hiyo, Al-Ittihad baada ya kumalizika kwa mkataba wake Chelsea, huku Mfaransa mwenzake, Karim Benzema naye pia alisaini katika klabu hiyo.