Beyonce ameweka rekodi mbili nzito kwenye tamasha kubwa la Coachella la mwaka huu alipopanda jukwaani Jumamosi, Aprili 14.
Kwanza, Bey amekuwa mwanamuziki wa kwanza mwanamke mweusi kuwa msanii kiongozi kwenye tamasha hilo tangu lilipoanzishwa.
Kazi kubwa aliyoifanya jukwaani ilisababisha afunike kila kilichokuwa kinaendelea, hali iliyosababisha tamasha hilo kubatizwa jina la muda la ‘Beychella’ badala ya Coachella.
Katika hatua nyingine, Malkia Bey aliweka rekodi kwenye YouTube baada ya ‘show’ yake kutazamwa moja kwa moja (streaming) na watu zaidi 458,000.
Hiyo ni idadi kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa kwa watu kuangalia YouTube moja kwamoja kupitia channel maalum ambayo inalipiwa na kuingiza fedha nyingi.
Bey alisaidia Coachella kuingiza kiasi kikubwa zaidi cha fedha kwenye historia yake kupitia YouTube, ikiangaliwa zaidi ya mara milioni 43.1 duniani kote kwenye mtandao huo.
Ndani ya saa mbili alizokuwa jukwaani, Bey alikuwa na watu zaidi ya 100 kwenye jukwaa ambao ni pamoja na madansa. Aliwapa shangwe zaidi mashabiki wake kwa kupanda na Destiny’s Child, mumewe Jay Z pamoja na ndugu yake Solange.